Tuesday 11 March 2014

NANI WA KUNUFAIKA NA MIKATABA YA WAWEKEZAJI WA NJE HAPA TANZANIA ?????

Kwanini wawekezaji wakubwa wa nje hapa Tanzania wanapewa sana misamaha ya kodi na serikali wakati wazawa kila siku wanazidi kubanwa katika kulipa kodi na serikali hiyohiyo??

Unakuta wawekezaji mfano, mahotel makubwa au makampuni mengine, wanaachiwa kwa miaka hadi 5 bila kulipa chochote, na serikali inasema inawapa mda waangalie kama kuna faida ama hasara na badala yake wakipata faida zao wanadanganya kuwa wamepata hasara ghafla na jina la kampuni linabadilishwa lakini ukija kuangalia kwa makini ni kampuni ileile na serikali inazidi kuingia hasara wakati wawekezaji haohao wanazidi kupata faida.

Kiuhalisia makampuni mengi sana ya nje yanayokuja kuwekeza hapa nchini Tanzania huwa yanapata faida tena sana ila ni kwakuwa kama nchi, haina sera nzuri juu ya uwekezaji ndio maana wanazidi kuitana ili kuinyonya nchi yetu.

Kwahiyo unakuta nchi au serikali inazidi kuwanufaisha wawekezaji wa nje na kuifanya Tanzania izidi kupoteza mapato na hatimaye kuzidi kuwa masikini.

Sera nyingi sana za uwekezaji haziwanufaishi wazawa bali ni wawekezaji wa nje.Mikataba mingi sana inayotiliwa saini,mfano madini, n.k,kwa asilimia nyingi sana huwa inazidi kuinyonya nchi.

Mwalimu Nyerere alishawahi kusema kuwa,madini sio kitu ambacho kinaweza kuharibika kisipochimbwa hata na kizazi kilichopo sasa,ni vyema watu wakasubiri yakabaki hukohuko ardhini ili kuwe na wataalamu wa kutosha ili yatakapochimbwa yaweze kuwanufaisha watanzania kuliko kufanya haraka katika kuyachimba na ikawa hasara kwa taifa la Tanzania.

Pia kuna wakati flani mh. Tundu Lissu kama mbunge na mwanasheria,akiwa kwenye mahojiano kwenye kipindi cha "Dakika 45" ambacho kinarushwa na kituo cha ITV,aliwahi kusema, hata wao kama wabunge hawapewi ruhusa ya kuiona hiyo mikataba inayofanyika baina ya wawekezaji pamoja na serikali.

Aliongeza na kusema kuwa,"ukihitaji mikataba yoyote ili kuipitia unaambiwa uombe kwa maandishi lakini kamwe hautakuja kuipata."

Sasa kama wawakilishi wetu kwamaana ya wabunge na bunge zima kiujumla likijumuisha watendaji mbalimbali wa wizara za serikali hawapewi nafasi wakiwa bungeni ya kujadili hiyo mikataba,ni nani wa kuirekebisha ikawa faida kwa taifa letu Tanzania lenye utajiri wa rasilimali na sio kwa watu wachache???

Nadhani hiki ni kipindi kizuri sana kwakuwa bado tupo kwenye mchakato wa kuipata katiba mpya swala hili nalo likawekewa mkazo.

Nashauri mikataba baina ya serikali na wawekezaji wa nje ijadiliwe bungeni ili wataalamu mbalimbali waweze kuichambua vizuri kwa mustakabali wa taifa letu Tanzania.

Pia elimu itolewe ya kutosha inayohusu mikataba hiyo kwa maana ya faida zake kwa wazawa sio tu kwa watanzania kiujumla bali hata kwa wazawa wa eneo mahususi linalowekezwa.

No comments:

Post a Comment