Wednesday 26 March 2014

WATUMISHI WA MUNGU WATUMIE PIA ELIMU YAO KUIKOMBOA JAMII.

Leo ndugu wadau nimeona niwape kisa ambacho natumai kwa watakao nielewa kitawasaidia.

Mahali flani kulikuwa na wanakijiji ambao maji yao yote ya kijiji hicho walikuwa wanayapata kwenye msitu mmoja ambao ulikuwa unapatikana kwenye kijiji hicho.

Ndani ya msitu huo inasemekana kuna nyoka mkubwa sana ambaye ndiye aliyesadikika kuwa ndiye chanzo chote cha maji ya kijiji hicho,kwahiyo wazee wa kijiji hicho walikataza kabisa mtu yeyote asije akakata mti ndani ya msitu ule maana watu wakiwa wanakata miti basi nyoka huyo atakasirika na kutotoa maji tena na huenda akahama kijiji hicho.
Miaka nenda rudi msitu huo haukukatwa mti kamwe na kuacha uoto wa asali wa msitu huo kuendelea kukua vizuri siku hadi siku.

Baada ya miaka kadhaa,mtumishi wa MUNGU aliweza kuhamia na kuanza kuishi ndani ya kijiji hicho.Kutokana na hali ya maji ya kijiji kile ilivyo na chanzo chake kama inavyosemekana kuwa ni yanaletwa na nyoka huyo mkubwa,mtumishi huyo hakupendezwa na hiyo hali kutokana na imani aliyonayo.Mtumishi huyo aliona haimpendezi kabisa kutumia maji hayo kwa vile inasemekana yanatolewa na nyoka wa msitu huo.

Mtumishi huyo aliona imefika wakati wa kutomtukuza nyoka huyo bali ni MUNGU pekee,kwahiyo aliwapa somo wanakijiji na wakapanga kwenda kukata miti yote iliyokuwa inapatikana ndani ya msitu huo ili kama sio kumuua huyo nyoka basi wamfukuze kabisa kwasababu ni roho chafu kulingana na imani yao na hapaswi kutukuzwa.

Wanakijiji wakishirikiana na mtumishi wa MUNGU waliweza kukata miti yoote ya msitu ule na kuona kuwa wameishinda nguvu hiyo ya giza.

Baada ya miaka kadhaa,kijiji hicho kikaanza kukosa maji kabisa,baada ya wazee na baadhi ya watu kukaa na kuwaza kwanini,jibu walilolipata ni kwamba mtumishi yule na watu alioshirikiana nao kukata miti ya msitu ndio chanzo cha ukosefu wa maji katika kijiji hicho.

Miaka ilizidi kwenda bila kijiji kupata maji na matokeo yake wanakijiji wakaamini kuwa ni kweli kwamba kufukuzwa kwa yule nyoka ndani ya msitu kulikosababishwa kukatwa kwa miti yoote ndio kumemfanya akasirike na kuwakosesha maji.

Mtumishi wa MUNGU hakujua lengo la wazee walioweka sheria hiyo walikuwa na maana kubwa sana.
Walijua miti ikikatwa itasababisha ukame na walifanya hivyo ili kuwatisha watu wakijua watatii na kutokata kabisa miti iliyopo ndani ya msitu huo.



Kama mtumishi wa MUNGU, unatumiaje elimu yako ya kiroho na kidunia katika kuwaelimisha na kuwakomboa wananchi kulingana na eneo ulilopo????


Tuesday 25 March 2014

TAARIFA KWA WALIMU WAPYA KABLA YA KURIPOTI KWENYE VITUO VYAO VIPYA VYA KAZI.

Ndugu wadau wa taaluma hii ya ualimu kwanza nipende kutoa pongezi kwa wale wote ambao wameweza kupangiwa vituo vyao vipya vya  kazi,haijalishi umepangiwa wapi na serikali ila kikubwa ni kupata nafasi ya kazi kwanza na mengine ndio yatafata baadae.

Pia napenda kutoa pole kwa wale wote ambao mpaka sasa hawajayaona majina yao ila bado wanayasubiri.Naomba mzidi kuwa na subira juu ya hilo ingawa inaumiza sana.

Leo nimeona ni vyema kuwapa taarifa muhimu wale wote ambao wamepata nafasi katika vituo vyao vipya vya kazi ya kufundisha.

Haya ni mambo muhimu yakuzingatia kabla hujaripoti kwenye kituo chako kipya cha kazi:

1.Mpaka sasa halmashauri nyingi zimeshatoa majina ya shule unayotakiwa kufundisha.Kwahiyo kwa wale wote ambao majina yao yalitolewa bila kuonesha umepangiwa shule gani,unaweza kuwasiliana na mtu yeyote aliye kwenye halimashauri husika akuchekie jina lako kwenye mbao za matangazo za hiyo halmashauri ili ujue umepangiwa shule gani.
Kama halimashauri yako hawajayaweka basi ni maswala yao tu ya utendaji huenda hayajakaa vizuri.



2.Kuna vitu vya kubeba ambavyo vinatakiwa kuwasilishwa kwenye shule husika,navyo ni kama vifuatavyo:

  • Cheti chako cha kuzaliwa.
  • Cheti chako cha kidato cha nne.
  • Cheti chako cha kidato cha sita kama utakuwa nacho maana kuna wengine waliunga diploma baada ya kumaliza certificate.
  • Cheti chako cha chuo pamoja na transcript. 

3.Pia unaweza kubeba picha za passport size za ndugu zako au watu wako wa karibu unaotaka watengenezewe vitambulisho vya bima ya afya.Maana huwa kwa kawaida ni watu 6 ukiwa na wewe.Kubeba passport zao mapema itakusaidia kuokoa gharama za kuzituma tena wakati zinapohitajika maana natumai utakuwa mbali nao.


Mwisho niwatakie kila lakheri katika utendaji wenu mpya wa kazi.

Sunday 23 March 2014

NI LINI VIONGOZI WA TANZANIA WATAACHA KUTIBIWA NJE YA NCHI ????

Kwa sasa Tanzania ina miaka 52 toka ipate uhuru wake.
Kwanini mpaka leo huduma muhimu za kijamii kama hospitali hazijaboreshwa ipasavyo na kufanya hata viongozi wengi wa nchi kwenda nje ya nchi kutibiwa??

Kwanini tusiige nchi kama ya Afrika ya Kusini, Mzee Mandela katibiwa na akafia hospitali iliyopo nchini kwake??

Lini huduma za afya zitaboreshwa??

Kama viongozi wenye dhamana hawaboreshi ipasavyo huduma za afya na kwenda nje ya nchi kutibiwa,sisi wananchi wa kawaida ndio pekee tutaendelea kukaa katika mazingira ambayo dawa na wataalam wa huduma za afya ni hadimu kupatikana????

Naomba kuwasilisha.











Thursday 20 March 2014

TUWE MAKINI NA MALEZI YA WATOTO.

Katika malezi ya familia yoyote,wazazi kwa maana ya baba na mama wana majukumu makubwa sana ya kuhudumia familia zao kwa kila hali kadiri wawezavyo.
Kama wazazi tena wanao wajali watoto wao,lazima wahakikishe watoto wao wanapata mahitaji muhimu ya kijamii kama chakula,malazi na makazi mazuri.

Lakini katika maswala yoote ya malezi kwa watoto,usafi pia ni swala muhimu sana.Kama mzazi/mlezi inakupasa uhakikishe mtoto au watoto unaowalea mda wote wanakuwa kwenye mazingira ya usafi.
Kuwaacha watoto kuwa wachafu kutasababisha magonjwa mengi sana kwenye miili yao na hatimae kuumwa na kuidhoofisha miili hiyo.

Vilevile,kutaweza kukusababishia gharama kubwa za matibabu pindi pale watakapoanza kuumwa.
Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba.

Licha ya hivyo uchafu huleta aibu kwenye jamii inayokuzunguka.Unapo waacha watoto wako wawe wachafu,usifikiri lawama zote zitakuwa kwao tu bali hata kwako mzazi/mlezi, maana utaonekana huwajali watoto wako na kuonekana hovyo mtaani.

Ifike mahali usafi wa miili na mazingira usiwe tu kwa wazazi/walezi pekee,bali hata kwa watoto wao wanao walea.



Sunday 16 March 2014

AJIRA ZA WALIMU WAPYA 2013/2014 HIZI HAPA

Ajira za waalimu wapya baada ya kusubiriwa saaana hatimaye zatolewa.

Soma hapa kuziona zoote kuanzia cheti,diploma,shahada na wale waliopangiwa kufundisha vyuoni


Fungua hapa

Saturday 15 March 2014

ZIJUE KEMIKALI ZINAZOPATIKANA KWENYE UVUTAJI WA SIGARA.

Ndugu wadau, leo nimeona niwaoneshe japo kidogo tu madhara yanayoletwa na uvutaji wa sigara.

Wataalamu wanasema moshi wake haumdhuru tu yule mvutaji bali hata anayepokea ule moshi wake.Kwamaana hiyo sigara ina madhara kwa mvutaji na hata mtu aliye karibu katika kuupokea ule moshi na kumuingia mwilini mwake.

Nipende kueleza kuwa ni vyema kwa mvutaji kuachana na sigara na hata mtu wa kawaida ambaye havuti kuwa mbali nayo,kwa maana ya moshi wake.

Kwa yeyote atakaye hitaji kuacha,nashauri aende kwenye vituo vya afya kuwaona wataalamu wa mambo haya naamini daktari atakupa njia sahihi ya kuachana na uvutaji wa sigara au tumbaku zozote za namna hii ili kuunusuru mwili pamoja na afya yako.

Hebu tazama jinsi sigara inavyokuwa na kemikali nyingi ambazo huleta sana sumu kwenye miili ya binadamu.















Thursday 13 March 2014

BODABODA,BAJAJI NA GUTA ZAPIGWA MARUFUKU JIJINI DAR ES SALAAM.

Wakihojiwa na TBC 1,Kamanda wa polisi bwana Sulemani Kova,Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam bwana Saidi Mecki Sadiki ,pamoja na Afisa Mfawidhi kanda ya mashariki,Conrad Shio wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) wameweza kuelezea jinsi mchakato huu utakavyokuwa jijini Dar es Salaam.

Wote waliweza kutoa sababu mbalimbali ya kwanini wameamua kushirikiana katika kuhakikisha vyombo hivi vya usafiri haviingii sehemu za mijini.

Vyombo hivi vya usafiri yaani bajaji,bodaboda na maguta ( baiskeli zenye matairi matatu) vitakatazwa kuingia sehemu zote za CBD (mijini).
Wakitolea mifano wa sehemu hizo ni,ukitokea Bunju hadi kuja Tegeta,mwisho wa vyombo hivyo utakuwa ni Mwenge

Pia ukitokea Mbezi ya Msuguli mwisho itakuwa Kimara kwahiyo ukija Ubungo utazuiliwa.
Kwahiyo maeneo yoote ya mijini Posta ikiwemo,vyombo hivi havitaruhusiwa kuingia


                                 SABABU ZA KUZUIWA KUINGIA.


Viongozi hawa watatu waliweza kutoa sababu mbalimbali za kwanini vyombo hivi vimekatazwa kuingia sehemu za mijini.
Sababu hizo ni kama zifuatazo


2.Kuzuia matukio ya ualifu yanayofanyika kwakutumia sana bodaboda.Yaani bodaboda zinatumika sana kwenye matukio ya uhalifu kama wizi na ujambazi.


3.Kuzuia msongamano wa vyombo vya usafiri jijini.


4.Kupunguza ajali zinazosababishwa haswahaswa na vyombo hivi mfano bodaboda.kamanda Kova alitolea mfano kuwa unakuta kijana wa bodaboda yupo mataa lakini hata kama taa hazijamruhusu yeye anapita na kuacha magari kubakia kwenye mataa.Hapa aliuliza kwani waliosimama sio watu????
Kwahiyo alisema vyombo hivi madereva wake wengi hawafati sheria za barabarani




                                                   HITIMISHO.

Walisisitiza kuwa vyombo hivyo vimeruhusiwa kwa shughuli za biashara pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.
Pia kwa wale watu wanaotumia kama usafiri wao binafsi yaani sio kibiashara wanaruhusiwa kuingia navyo mijini hususani pikipiki kwa sharti la kuwa pekee yaani bila kumpakiza mtu nyuma.

Kamanda Kova aliongeza na kusema,kama mtu akitoka pembezoni mwa mji mfano Bunju au Tegeta basi akifika Mwenge ambapo ndio mwisho wa bodaboda za biashara, atatakiwa achukue usafiri wa umma na kuendelea na safari zake.


Kamanda Kova alisema kama sheria inatakiwa itende haki kotekote maana kuna watu wanaweza kudanganya kuwa pikipiki anayoiendesha siyo ya biashara kwahiyo mtu aliyembeba ni rafiki au mpenzi wake na ikachukuliwa kawaida lakini itaonekanaje kwa wale wafanya biashara wanaopakiza nao watu kama hawa???
Kwahiyo sharti ni uwe mwenyewe kwenye pikipiki yako.


Naye Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Conrad Shio ameeleza kuwa sheria ya usafirishaji kusimamia Bajaji na Bodaboda iko wazi na kuongeza kuwa serikali ina wajibu wake na pia waendesha pikipiki na Bajaji wanawajibu wao wa kuzingatia kanuni taratibu na kanuni zilizowekwa.

“Sisi kama SUMATRA tunaendelea kufanya kila tuwezalo kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjivu wa sheria za barabarani”




Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Conrad Shio akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu sheria inayosimamia usafiri wa Bajaji na Bodaboda nchini.





Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna (CP) Suleiman Kova akitoa ufafanuzi ameeleza kwa waandishi wa habari kuhusu wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria za barabarani na kajenga tabia ya kufanya tathmini ya safari zao iwapo wanakidhi vigezo vya usalama barabarani ili kuepusha madhara.




Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kutoa agizo kwa viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanawaondoa na kuwachukulia hatua za kisheria wanaovunja sheria za jiji kwa kuendesha shughuli mbalimbali katika maeneo yasiyoruhusiwa.

MATAPELI VYUONI WAZIDI KUJA NA MBINU MPYA

Nimeona leo nilete habari hii kwasababu naamini itaweza kuwasaidia wadau wengi sana.

Kwa sasa nchini kwetu Tanzania ukosefu wa ajira unazidi kuchukua kasi na sio tu kwa ambao wanaonekana hawana elimu bali hata wale wenye vyeti mbalimbali vya chuo kwa ngazi mbalimbali kama cheti,astashahada na shahada.

Kwa sasa Tanzania ina idadi ya watu zaidi ya milioni 45,kwamaana hiyo idadi ya ongezeko la watu kila siku yazidi kuongezeka tofauti na miaka ya zamani.

Ongezeko hili la watu linafanya watu wengi sana kuona fursa za kuwa na maisha mazuri zipo mijini tu na kuondoka sehemu zao hususani vijijini wakiamini wakiwa huko hawatapata fursa za mafanikio ambacho hicho kitu kwangu mimi naona hakipo sahihi na naamini popote pale fursa zinaweza kupatikana na sio mijini tu.

Kutokana na ukosefu mkubwa wa ajira, kuna wengine  wameamua kujipatia pesa kwa njia ambazo sio za halali yaani kuwadanganya watu kuhusu mambo flaniflani ambao hao ndio wanaoitwa MATAPELI.

Naomba nitoe mfano ambao umenitokea mimi mwenyewe hivi karibuni:

Mimi nilibahatika kumaliza shahada ya ualimu na sanaa (bachelor of education arts) katika chuo kikuu cha Tumaini tawi la Iringa mwaka jana 2013.Taaluma niliyosomea huwa tunapangiwa ajira na serikali (posts),lakini huwa napenda sana kuwa Tutorial Assistant (Kufundisha chuoni), kwahiyo nikaona ni bora nitume maombi kwenye vyuo ili nifanye ninachokipenda zaidi.

Niliweza kutuma maombi katika vyuo mbalimbali hapa nchi kwetu huku nikiendelea kusubiri majibu.

Hivi karibuni nilipigiwa simu na waliojiita wafanyakazi wa chuo kimoja cha serikali kilichopo pale Kigamboni hapa Dar es Salaam, ambapo ilikuwa jumamosi ya wiki iliyopita kwamba wameona CV yangu na wakawa wanaisoma mbele yangu kupitia simu.Mtu wa kwanza aliniambia kuwa yeye anatoka kwenye idara ya Data Base na akaniambia nimpigie kiongozi wake ili anipe ratiba zote za interview.

Nilipompigia huyo mtu wa pili alinieleza kuwa nina vigezo vyote vya kufanya kazi nao na aliniambia nije alhamisi yaani leo tarehe 13/3/2014 nikiwa na passport size 4,ila wao kama chuo huwa wana utaratibu wao kwa wafanyakazi wapya yaani unatakiwa kulipia gharama ya elfu 35,800 kwaajili ya usajili wa mambo mbalimbali ya hapo chuoni.Na fedha hizo natakiwa nije nazo siku hiyo ya interview.

Pesa hiyo ilinishtua mara ya kwanza na kumuhoji kuwa inakuwaje interview unatakiwa kulipia????

Alichonijibu ni kuwa hulipii interview na hamna sehemu yoyote ya malipo hayo ila hiyo pesa ni kwaajili ya usajili wa mambo kadhaa ya hapo chuoni.

Mimi binafsi nilianza kutilia mashaka juu ya kazi hiyo na kuamua kufanya uchunguzi wangu kabla ya siku hiyo kufika.
Uchunguzi niliufanya kwakushirikiana na baba yangu.Yeye alikwenda pale chuoni na kuanza kuhoji kwanza kuhusu uwepo wa hao wafanyakazi wawili.

Niliamua kumuomba mzee aende ili iwe rahisi kuwagundua ili kama hautakuwa udanganyifu basi wasiweze kunitilia mashaka siku hiyo ya interview.

Mzee wangu alipofika pale aliweza kuingia idara mbalimbali na kuhoji pasipo kunitaja jina juu ya utaratibu woote wa wafanyakazi wapya na uwepo wa hao wafanyakazi.Lakini idara zote alizoingia walimwambia kama chuo cha serikali hakina utaratibu huo na mara nyingi utumishi ndio wanaleta watu ingawa hata chuo kina nafasi yake.
Na katika interview lazima kuwepo na afisa wa utumishi pamoja na watendaji wengine wa hapo chuoni.Vilevile hakuna malipo yoyote mtu atatakiwa kulipia kwaajili ya interview.
Mwisho walimaliza na kusema kuwa hao ni matapeli tena wanatakiwa wakamatwe.

Baada ya majibu hayo nilijaribu kuwatafuta wale wahusika siku ya jana na leo ili niwasikilize zaidi watasemaje,kiukweli mpaka sasa kila nikimbana kwa maswali yule mkubwa wao anajifanya yupo bize sana na akisema atanipigia yupo bize kidogo,na amefanya hivyo zaidi ya mara 4.
Na mapaka sasa hawajanitafuta tena.

Hapo ndipo nilidhibitisha kuwa hawa ni matapeli wanaotumia fursa ya watu wanaotafuta kazi hususani vyuoni kuwalaghai.

Nitoe angalizo kwa yeyote anayetafuta kazi,anatakiwa awe makini sana na interview.Ukiambiwa unatakiwa kulipa gharama flani ili upate kazi ujue hapo huenda kukawa na utapeli, kwahiyo unatakiwa ufanye uchunguzi mkubwa binafsi kabla ya siku hiyo.

Wednesday 12 March 2014

MATOKEO YA MWENYEKITI WA KUDUMU WA BUNGE LA KATIBA YATANGAZWA.

Msimamizi wa uchaguzi wa mwenyekiti wa bunge maalumu la katiba,ameweza kutangaza matokeo ya mwenyekiti wa kudumu wa bunge hilo.

Katika mchuano huo walikuwa wagombea wawili ambaye wa kwanza ni Mh. Samweli John Sitta pamoja na Mh. Hashim Rungwe.

Katika uchaguzi huo,

Kura zilizopigwa ni 629

Wapiga kura wote walikuwa 563

Zilizoharibika ni 7

Katika kura hizo Mh. Hashim Rugwe alipata kura 69 na Samwel Sitta alipata kura 487.

Kwa matokeo hayo Mh. Samweli Sitaa kaibuka na ushindi wa kuwa mwenyekiti wa kudumu wa bunge maalumu la katiba.

Mh. Samweli Sitta atapokea kiti hicho kutoka kwa mwenyekiti wa muda wa bunge maalumu la katiba, mh. Pandu Amir Kificho.

Katika pongezi zake mh. Sitta ameahidi utendaji kazi kwa uadilifu na kasi.


UCHAGUZI WA MAKAMO MWENYEKITI WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA.

Katika upande mwingine,mwenyekiti wa muda wa bunge maalumu la katiba,mh. Pandu Amir Kificho,ameweza kutoa ratiba ya uchaguzi wa makamo mwenyekiti wa bunge maalumu la katiba utakaofanyika kesho tarehe 13/4/2014, saa 10 jioni.

Katika sheria iliyopo sasa inasema mwenyekiti akitokea Bara basi makamo wake anatakiwa atokee Zanzibar.Pia kama mwenyekiti atakuwa mwanaume basi makamo wake anatakiwa awe mwanamke.

Na uchaguzi uliomalizika leo na kumfanya Mh. Samweli Sitta kuwa mshindi,utafanya kwa sasa makamo wake awe mwanamke na atokee Zanzibar.

Fomu za kugombea zitatolewa leo mara baada ya kikao cha bunge kuisha kwenye ofisi ya baraza la wawakilishi.

Mgombea yeyote anatakiwa awe na wadhamini wasiopungua 20 yaani 10 kutoka bara na 10 wengine kutoka Zanzibar. 

Fomu zote zitatakiwa kurudishwa kesho sa 4 asubuhi kwenye ofisi hizohizo.



sitta

Tuesday 11 March 2014

NANI WA KUNUFAIKA NA MIKATABA YA WAWEKEZAJI WA NJE HAPA TANZANIA ?????

Kwanini wawekezaji wakubwa wa nje hapa Tanzania wanapewa sana misamaha ya kodi na serikali wakati wazawa kila siku wanazidi kubanwa katika kulipa kodi na serikali hiyohiyo??

Unakuta wawekezaji mfano, mahotel makubwa au makampuni mengine, wanaachiwa kwa miaka hadi 5 bila kulipa chochote, na serikali inasema inawapa mda waangalie kama kuna faida ama hasara na badala yake wakipata faida zao wanadanganya kuwa wamepata hasara ghafla na jina la kampuni linabadilishwa lakini ukija kuangalia kwa makini ni kampuni ileile na serikali inazidi kuingia hasara wakati wawekezaji haohao wanazidi kupata faida.

Kiuhalisia makampuni mengi sana ya nje yanayokuja kuwekeza hapa nchini Tanzania huwa yanapata faida tena sana ila ni kwakuwa kama nchi, haina sera nzuri juu ya uwekezaji ndio maana wanazidi kuitana ili kuinyonya nchi yetu.

Kwahiyo unakuta nchi au serikali inazidi kuwanufaisha wawekezaji wa nje na kuifanya Tanzania izidi kupoteza mapato na hatimaye kuzidi kuwa masikini.

Sera nyingi sana za uwekezaji haziwanufaishi wazawa bali ni wawekezaji wa nje.Mikataba mingi sana inayotiliwa saini,mfano madini, n.k,kwa asilimia nyingi sana huwa inazidi kuinyonya nchi.

Mwalimu Nyerere alishawahi kusema kuwa,madini sio kitu ambacho kinaweza kuharibika kisipochimbwa hata na kizazi kilichopo sasa,ni vyema watu wakasubiri yakabaki hukohuko ardhini ili kuwe na wataalamu wa kutosha ili yatakapochimbwa yaweze kuwanufaisha watanzania kuliko kufanya haraka katika kuyachimba na ikawa hasara kwa taifa la Tanzania.

Pia kuna wakati flani mh. Tundu Lissu kama mbunge na mwanasheria,akiwa kwenye mahojiano kwenye kipindi cha "Dakika 45" ambacho kinarushwa na kituo cha ITV,aliwahi kusema, hata wao kama wabunge hawapewi ruhusa ya kuiona hiyo mikataba inayofanyika baina ya wawekezaji pamoja na serikali.

Aliongeza na kusema kuwa,"ukihitaji mikataba yoyote ili kuipitia unaambiwa uombe kwa maandishi lakini kamwe hautakuja kuipata."

Sasa kama wawakilishi wetu kwamaana ya wabunge na bunge zima kiujumla likijumuisha watendaji mbalimbali wa wizara za serikali hawapewi nafasi wakiwa bungeni ya kujadili hiyo mikataba,ni nani wa kuirekebisha ikawa faida kwa taifa letu Tanzania lenye utajiri wa rasilimali na sio kwa watu wachache???

Nadhani hiki ni kipindi kizuri sana kwakuwa bado tupo kwenye mchakato wa kuipata katiba mpya swala hili nalo likawekewa mkazo.

Nashauri mikataba baina ya serikali na wawekezaji wa nje ijadiliwe bungeni ili wataalamu mbalimbali waweze kuichambua vizuri kwa mustakabali wa taifa letu Tanzania.

Pia elimu itolewe ya kutosha inayohusu mikataba hiyo kwa maana ya faida zake kwa wazawa sio tu kwa watanzania kiujumla bali hata kwa wazawa wa eneo mahususi linalowekezwa.

Saturday 8 March 2014

KWANINI BADO WANAFUNZI WANAKAA CHINI BILA MADAWATI?????

Licha ya Tanzania kuwa na misitu mingi yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha mbao, bado wananchi wake hawanufaiki nayo vyakutosha/ipasavyo.

Hii inapelekea hata wanafunzi wake kwa kiasi kikubwa katika shule nyingi kukosa madawati na kukaa chini toka uhuru mpaka sasa ambapo nchi yetu Tanzania imefikisha miaka 52 toka ipate uhuru.


NINI MAONI YAKO??













ZIFUATAZO NI PICHA ZA SHULE YA MSINGI ETARO ILIYOPO MUSOMA VIJIJINI












Wanafunzi wakiendelea na masomo yao huku wengine wakitumia magoti yao kama sehemu za kuandikia huku wakiwa wamekaa chini.





Hali halisi ndiyo hii wilayani Musoma vijijini





Friday 7 March 2014

MAPAMBANO DHIDI YA MOJA WA ADUI WA TANZANIA BADO HAYARIDHISHI.

Ndugu wadau wa blog hii,nilishawahi kupost habari hii,kupitia PAGE yangu iitwayo "Save Societies" iliyopo facebook mda mrefu lakini nimeamua kuileta tena ili watu ambao hawakupata fursa kuipitia waweze kuisoma.

Tanzania ina maadui wakubwa 3,ambao ni UJINGA,UMASIKINI na MARADHI.

Hapa nimeamua kumuonesha adui mmojawapo anaesumbua sana nchi yetu ya Tanzania.

Hebu karibu usome ili unielewe zaidi.



Katika hali isiyo ya kawaida,shule moja wilayani Bagamoyo imekutwa ikiwa na mwalimu mmoja tu
anayefundisha wanafunzi kuanzia chekechea hadi darasa la saba,wote wakifundishwa katika chumba
kimoja kwa kutumia ubao mmoja.

Hata hivyo,katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana,wanafunzi wote 12 walifaulu kuingia kidato cha kwanza.
Shule hiyo ya msingi Machala, iliyokuwa na idadi ya wanafunzi 198 imejengwa kwa majani kuanzia
chini hadi kwenye paa.

Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea shule hiyo, alimkuta mwalimu huyo akiwafundisha wanafunzi hao wa madarasa tofauti wakiwa kwenye chumba kimoja,huku ubaowakufundishia ukiwa umechorwa
mistari mitatu kutenganisha masomo ya chekechea hadi darasa la pili,mstari mwingine darasa la tatu hadi la tano na mwingine darasa la sita hadi la saba.

Mwalimu huyo,Christopher Rukutu,aliliambia NIPASHE kuwa shule hiyo hutumia kivuli cha mti kama ofisi.

Shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Mihunga Kata ya Miono,Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani,ilianzishwa na serikali tangu mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 12 ambao wamemaliza darasa la saba,mwaka jana na kubahatika kufaulu wote.

Kwa mujibu wa mwalimu Rukutu,wanafunzi wote waliofaulu walipata alama za A na B isipokuwa mmoja aliyepata alama C.

Pamoja na kuwa katika mazingira magumu,shule hiyo kiwilaya ilishika nafasi ya sita na kimkoa nafasi ya 20.

Alisema shule hiyo haina vitabu vya kiada wala vya kufundishia na amekuwa akiazima kutoka shule za jirani.

SOURCE: NIPASHE

NINI MAONI YAKO???








Tuesday 4 March 2014

KADINALI PENGO ATOA MSIMAMO WAKE BINAFSI KUHUSU MFUMO WA KUPIGA KURA KWENYE BUNGE LA KATIBA

Akiongea leo na waandishi wa habari,tarehe 4~3~2014,Askofu Mkuu wa kanisa katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo amesema kama kanisa halijasema chochote kuhusu mfumo wa serikali kama linavyozushiwa kuwa,kanisa la katoliki linataka serikali mbili ndio ziwepo.
Amesema huo sio msimamo wa kanisa na wala kanisa halijasema chochote kuhusu hilo swala.

Kwa upande mwingine,Kadinali Pengo amegusia kuhusu swala la upigaji kura unaotakiwa kutumika katika bunge la katiba linaloendelea hapa nchini Tanzania,mkoani Dodoma.Ili kueleweka zaidi aliamua kutoa mfano huu,

"Mimi nikiwa na bosi wangu na likaulizwa swali,lazima nimwache bosi wangu anyooshe kidole kwanza na kujibu ili mimi nifuate,maana kama nitakuwa tofauti nae,nitahofia kupoteza kazi yangu ofisini.Kwahiyo mimi binafsi na siyo kama kanisa,napendekeza mfumo wa kura ya siri utumike."

Alisema Kadinali Pengo akiongea na waandishi wa habari.





SOURCE: ITV

Sunday 2 March 2014

WAZUNGU WAZIDI KUSAMBAZA LAANA ZAIDI YA SODOMA NA GOMORA.

Wazungu wanapinga sana mwanaume akioa mke zaidi ya mmoja.Yaani kwao wanaona ni haramu sana kuruhusu hilo kwa wanaume.
Lakini cha ajaabu ni kwamba wanaruhusu ndoa za jinsia moja mfano mwanaume kumuoa mwanaume au mwanamke kumuoa mwanamke mwenzie.

Ndoa hizo za jinsia moja zinawezwa kufungishwa makanisani au taasisi zingine zinazohusika na zikaonekana za kawaida sana kwao.
Sasa kama mwanaume kuoa mke zaidi ya mmoja kwa wazungu sio sahihi na wanapinga sana hili,kwanini waone sahihi na kuruhusu ndoa za jinsia moja??

Kama ndoa ya mke zaidi ya mmoja,kanisa au taasisi nyingi za kwao haziwezi kupitisha,yaani mwanaume akawa na wake wawili woote kwa wakati mmoja,kanisa halitaweza kukubali na kufungisha ndoa hiyo maana itaonekana kinyume na taratibu,sasa iweje ndoa za jinsia moja zikubaliwe na kanisa au taasisi hiyohiyo??

Ukienda kwenye maandiko aidha ya biblia au Quran,MUNGU hajaruhusu kabisa ndoa za jinsia moja,sasa hawa wazungu na wote wanazozitetea wanafungisha kwakupitia maandiko gani???

Mnaita haki za binadamu,kwanini ndoa za mke zaidi ya mmoja nazo mnazikataa,na hamsemi kuwa ni haki za binadamu bali kwa Africa inaonekana kwamba ndio tuna maadili potofu???

Hizi ni zaidi ya laana za Sodoma na Gomora maana kipindi kile zilikuwa zaidi miji hiyo miwili lakini sasa ndoa za jinsia moja zinapigiwa debe zienee dunia nzima kwa kisingizio kwamba ni haki za binadamu.

Tanzania tunajipangaaje kukataa ndoa hizi???



ANGALIA PICHA ZA KUSHANGAZA ZA NDOA YA JINSIA MOJA KWELI DUNIA IMEKWISHA.




Mashoga na Wasagaji wamefunga ndoa iliyoshuhudiwa na mamia ya watu katika Kisiwa cha Rhodes Island na Minnesota nchini Marekani.


UKISTAAJABU YA MUSA, UTAYAONA YA FIRAUNI


Ripoti mbalimbali Agosti Mosi mwaka jana nchini Marekani, zinasema kuwa kwa sasa nchini Marekani zaidi ya robo ya Wamarekani wanaunga mkono ndoa za jinsia moja na makanisa mbalimbali yameingia na kuendelea kufungisha ndoa za aina hiyo.