Thursday 20 February 2014

Wakati wabunge wanazidi kupeta,wanataaluma wanazidi kudhalilika kimaslahi

Wakati wabunge wakiendelea kuongezewa posho za vikao, imebainika kuwa fedha anazolipwa mbunge mmoja kwa mwezi ni sawa na mishahara ya mwalimu wa shule ya msingi ya miaka mitatu. Malipo hayo pia yanaonekana kuwa sawa na mshahara wa mwaka mmoja wa daktari msaidizi mwenye shahada moja, anayeanza kazi.
 

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi umebaini kuwa mbunge mmoja hulipwa Sh 7.3 milioni kwa mwezi, ikiwa ni jumuisho la mshahara na malipo mengine ikiwamo posho za vikao. Jumuisho hilo ni pamoja na posho mbalimbali kila mwezi kama vile za mafuta ya magari, ubunge, kukaa jimboni, kuendesha ofisi na simu. Posho ya mafuta ni Sh 2 milioni kwa mwezi ikikadiriwa kuwa atatumia lita 1,000 ambazo makisio ni Sh2,000 kwa lita moja. Nyingine ni posho ya kukaa jimboni Sh 800,000, posho ya ubunge Sh1 milioni, kuendesha ofisi Sh 700,000, simu Sh 500,000 na mshahara ni Sh 2.3 milioni.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wakati mbunge akiwa hayupo bungeni inaelezwa bado analipwa posho hizo pamoja na mshahara na kumfanya ajikusanyie Sh 7.3 milioni kila mwezi. Wakati wa vikao bungeni, posho zao huongezeka ambazo uchunguzi unaonyesha mbunge hupewa posho nyingine za aina tatu; za kikao, kujikimu na usafiri.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, posho hiyo ya usafiri hupewa bila kujali kuwa ana posho ya kila mwezi ya mafuta ya Sh 2 milioni. Viwango vya fedha kwa posho anazopewa mbunge anapokuwa Bungeni kila kikao kwa sasa imeongezeka kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 ya posho ya kujikimu Sh 80,000 na usafiri Sh 50,000.


Mwalimu Lakini, wakati wabunge wakifurahia neema hizo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, mshahara wa mwalimu wa shule ya msingi anayeanza kazi, ambaye yupo kwenye daraja la mshahara la TGTS B ni Sh 200,000 kwa mwezi.


Kwa mwalimu wa sekondari mwenye stashahada ambaye yupo kwenye daraja la TGTS C, mshahara wake ni Sh 300,000 huku yule mwenye shahada wa daraja TGTS D analipwa Sh 400,000, mishahara yote ikiwa ni ya kuanza kazi.


Mchanganuo huo unaonyesha kwamba, pia viwango hivyo vya mshahara vilivyoorodheshwa hapo, ni vile ambavyo havijakatwa kodi zozote zile.Kutokana na hali hiyo, mapato ya Mbunge kwa mwezi mmoja yanaweza kumlipa mwalimu mmoja wa shule ya msingi mishahara ya miezi 36 sawa na miaka mitatu.

Mshahara huo pia utaweza kumlipa mwalimu mmoja wa sekondari mwenye stashahada mshahara wa miezi 24, huku yule mwenye shahada akilipwa kwa muda wa miezi 18 kwa mapato ya mwezi mmoja ya mbunge. Fedha hizo zinaweza kumlipa mfanyakazi wa idara nyingine ya umma, ambaye mshahara wake upo kwenye daraja hilo kwa kipindi kama hicho.



MAONI BINAFSI.


Wabunge wetu hapa nchini mishahara yao na posho havitegemei uzoefu wao wa kukaa bungeni kama watumishi wengine wa serikali,mfano WALIMU.Wabunge wamekuwa wakilipwa mishahara sawa hata kama ndio umeingia leo bungeni basi utapokea milion 7.3 kama wenzako uliowakuta kazini ambao walianza miaka mingi iliyopita.

Yaani kupanda kwa mishahara ya walimu kunategemea pia uzoefu alionao kazini na hata kupanda grade yake.Kadiri anavyopanda grade ndivyo mshahara wake unaongezeka.


SWALI
 

  • Kwanini kama UALIMU wanasema ni wito na UBUNGE usiwe hivyo???
  • Kwanini pia kazi ya UBUNGE mishahara yake isiendane na kupanda grade kama kazi ya ualimu au sekta zingine za serikali???

NB:
 

Kama nchi, ifike mahali tuamue kuwalipa vizuri wana taaluma mfano waalimu,madaktari n.k, kuliko wanasiasa.
 

Haiwezekani mtu mwenye taaluma mfano, ya Ualimu au Udaktari anapokea mshahara mdogo sana kuliko mwanasiasa ambaye unakuta ni "darasa la saba au form four failure".Huku ni kuzalilisha sana wanataaluma na kuudharau mchango wao mkubwa kwa mustakabali wa taifa letu.

Kuwapunguzia mishahara pamoja na posho wabunge na wanasiasa kwa ujumla inaweza ikasaidia kazi hiyo ikawa ya wito kama wanavyoitwa waalimu.Pia itasaidia kupunguza wimbi la watanzania wengi kukimbilia kwenye siasa kwa sasa.







No comments:

Post a Comment